KIVIPI FASIHI SIMULIZI NI MAMA WA FASIHI ANDISHI?
Ngure(2003) anasema kuwa fasihi ni aina ya sanaa ambayo
wasanii wake huonyesha ustadi wao katika kutumia maneno kisanii ili kuwasilisha
ujumbe wao kwa wasomaji au jamii iliyonuiwa.
Naye Mulokozi(1989) anasema, fasihi ni sanaa itumiayo
lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii bila kujali kuwa imeandikwa au
haijaandikwa.
Kwa ujumla fasihi ni aina au kazi ya sanaa ambayo hutumia lugha katika
uwasilishaji wake kwa hadhira lengwa ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa bila
kujali kuwa imeandikwa au haijaandikwa.
Mulokozi(1996) anasema kuwa fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa
kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na matendo bila kutumia
maandishi.Na anadai kuwa fasihi simulizi ni tukio linalofungamana muktadha au
mazingira Fulani ya jamii.
TUKI(2004)Fasihi simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa
kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa nji aya mdomo kama vile hadithi,ngoma na
vitendwili.
Kwa ujumla
fasihi simulizi ni ile kazi ya fasihi inayotungwa na kubuniwa katika kichwa cha
binadamu na kuwasilishwa kwa hadhira au jamii lengwa kwa njia ya masimulizi ya
mdomo na vitendo bila ya maandishi.
Wamitila(2003) anasema fasihi andishi ni sanaa itumiayo maandishi kufikisha
ujumbe kwa hadhira iliyo kusudiwa.
Hivyo basi fasihi andishi ni aina au kazi ya sanaa ambayo hutumia maandishi
kama njia kuu ya kufikisha ujumbe kwa jamii au hadhira lengwa iliyokusudiwa.
Ni kweli
na dhahiri kwamba fasihi simulizi ni mama wa fasihi andishi.Na hii ni kwa kuwa
fasihi simulizi ndiyo ya mwanzo kuibuka kwani hii ilianza mara tu binadamu
alivyoanza kupambana na mazingira yake.Fasihi ya kipindi cha mwanzo
ilijikita hasa katika masuala ya uzalisahaji mali ambapo nyimbo ziliimbwa ili
kuchapuza kazi.Fasihi andishi iliibuka mara tu binadamu alivyogundua maandishi
ndipo kazi mbalimbali za fasihi zilipoanza kuandikwa.Dai la kuwa fasihi
simulizi ni mama wa fasihi andishi linathibitishwa na hoja zifuatazo:-
Kwanza, dai hili linajidhihirisha katika tanzu za fasihi;tanzu za fashi
simulizi zinafanana sana na zile za fasihi andishi.Hii ni kwa kuwa fasihi
andishi imejichotea tanzu na vipera vyake katika fasihi simulizi.Mfano utanzu
wa hadithi fupi.Hadithi fupi andishi zimetokana na hadithi fupi
simulizi.Wanafasihi wengine wanauona utanzu huu kuwa ni wa fasihi simulizi kama
vile Kingei na Catherin(2010:3) kama wanavyonukuliwa na
samweil(2012:3).Samwel(2012:6),yeye anauchukulia utanzu huu wa hadithi fupi
kuwa ni utanzu wa hadithi fasihi simulizi na pia andishi.Hivyo basi utanzu wa
hadithi fupi andihshi umetoka na utanzu mmja wa fasihi andishi ambao ni utanzu
wa masimulizi.
Sio hayo tu,vilevile mitindo ya kazi fasihi simulizi;mtindo ni namna mwandishi
anavyoumba kazi yake.Ngure(2003) anasema kuwa `tunaweza kutumia mfano wa
Shaaban Robert katika kusadikika na kufikirika katika mitindo ya ngano zetu za
`paukwa –pakawa ‘wakaishi raha mstarehe’.Ngule anasema kuwa hadithi hizi zinamtiririko
mwepesi wa vituko uliofungamana na adili ya hadithi zenyewe.Mtindo huu niwa
kifasihi simulizi.Hivyo basi,Shaaban Robert ametumia mtindo wa fasihi simulizi
katika kuunda kazi yake ya fasihi andishi.Kwa maana hiyo fasihi andishi
imechukua muundo wa fasihi simulizi.
Vilevile suala la dhamira;dhamira ni kusudio la mtunzi wa kazi ya fasihi.
Ngure(2003)anasema kuwa dhamira nyingi wanazozijadili waandishi wa leo
zilikwishajadiliwa zamani katika fasihi simulizi.Na miongoni mwa dhamira hizo
ambazo Ngure anazitaja ni pamoja na mapenzi,kisasi,harakati za kitabaka na
unyonge wa mwanamke.Hii ni dhahiri kwamba dhamira za fasihi andishi zimetoka
katika zile za fasihi simuizi.Ngure anaendelea kwa kusisitiza kuwa fasihi
andishi haijafumbua dhamira mpya kabisa ila inaongezea maudhui mapya katika
dhamira zizo hizo.
Vilevile kipengele cha wahusika wa wao;hawa ni wanyama,vitu,miti,watu na
viumbe wengine ambao hubeba hulka na matendo ya binadamu.Wahusika ambao
wanatumika katika fasihi simulizi ndio haohao wanaotumika katika fasihi andishi
na kuwapa uhusika unaosawili matendo mbalimbali ya binadamu.Mfano hadithi za
sungura kama Samweli(2012:20) anavyonukuu hurafa ya sungura na mkulima kutoka
kwa Kanuri na wenzake(hakuna tarehe).Wahusika wake ni wanyama ambao hupewa
uwezo wa kutenda kama binadamu ili kueleza hali halisi.Wahusika hawa
wameingizwa katika kazi fasihi andishi.Wahusika kama watu hutumika katika
fasihi simulizi na ndio hao hao wanaotumika sasa katika fasihi andishi.Hivyo ni
dhahiri kwamba wahusika wa fasihi andishi wametokana na wahusika wa fasihi
siumlizi.
Hata hivyo muundo wa kazi hizo;muundo ni mtiririko na mpangilio wa visa na
matukio katika kazi ya fasihi.Hurekelea msuko wa visa na matukio katika fasihi.
Mara nyingi fasihi simulizi hutukia muundo wa moja kwa moja au muundo
sahili.Mfano hadithi nyingi kama hekaya za Abunuwasi (Samwel 2012:21) zina
muundo wa moja kwa moja.Yaani kisa huelezwa moja kwa moja bila kurejea nyuma au
kurukia matukio.Fasihi andishi imechukua muundo huu wa moja kwa moja katika
kuunda visa na matukio..Mfano Haji Gora Haji ametumia muundo wa moja kwa
moja katika riwaya yake ya Vuta n’Kuvute.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni